Social Icons

NIFA AD

NIFA AD

NIFAAAA

NIFAAAA

Thursday, July 15, 2021

KAULI YA WARIOBA YAIBUA HOJA KWA WASOMI JULLY 15,2021.

 


Dar es Salaam. Kauli ya Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kwamba Katiba Mpya ni kipaumbele kikubwa imewaibua wasomi na viongozi wa dini ambao wametoa maoni tofauti, baadhi wakimuunga mkono na wengine wakieleza mbinu mbadala.

Warioba alitoa kauli hiyo juzi usiku kwenye mahojiano yake na Kituo cha televisheni cha ITV wakati akizungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya Katiba.

Kauli yake imekuja wakati kuna vuguvugu la mabadiliko ya katiba kutoka kwenye vyama vya siasa, wanaharakati, viongozi wastaafu na wananchi mbalimbali ambao wana kiu ya kupata Katiba Mpya.

Kwa upande wa vyama vya siasa, Chadema imebeba ajenda ya kudai Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ujao wa mwaka 2025.

Julai 4, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema alikoleza mjadala huo aliposema hoja ya kutaka mchakato wa Katiba Mpya urejewe lisipuuzwe, bali pande mbili za wanaotaka na wasiotaka, wote wapewe nafasi.

Hata hivyo, Juni 28 wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka Watanzania wampe muda aimarishe uchumi wa nchi ili aweze kuangalia suala la Katiba Mpya na mikutano ya hadhara ambayo kwa sasa imezuiwa.

     ALICHOELEZA JAJI WARIOBA.

Katika mahojiano na ITV, Warioba alisema mtu yeyote anayekuwa madarakani anaapa kulinda na kuitetea Katiba kwa sababu ndiyo sheria mama.

“Unabadili sheria nyingi. Kila Bunge likikutana linabadili sheria nyingi, hii tunajua kwamba kuna mabadiliko yanahitajika, unawezaje kusema si kipaumbele? Tunaongozwa na nini katika nchi hii kama si Katiba?

“Katiba ni kipaumbele kikubwa kabisa. Nakubali kwa mazingira ya sasa lazima tuwe waangalifu, tunaikamilisha lini lakini tusije tukasema Katiba haina umuhimu,” alisema Jaji Warioba kwenye mahojiano hayo.

Hata hivyo, Warioba, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema Katiba bora haimaanishi kwamba matatizo yote yatakwisha, bali uadilifu na uaminifu ndio utaondoa matatizo mbalimbali yaliyopo, ikiwemo kupata Tume Huru ya Uchaguzi.

Akizungumzia maoni hayo alipohojiwa na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema anapozungumza Warioba kuhusu Katiba, anamaanisha, kwa sababu ni mtaalamu wa sheria na amewahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo ana uzoefu.

Alisema namna siasa za Tanzania zinavyofanyika, zinahitaji mwongozo mkuu wa Katiba ambao una uwiano sawa katika masuala mbalimbali.

“Kwa kila namna, kisiasa, kijamii na kiuchumi na kiteknolojia, Katiba Mpya inahitajika. Mazingira yote tuliyonayo yanahitaji uwepo wa Katiba Mpya na viashiria vinaonekana,” alisema.

Dk Loisulie ambaye ni msomi wa sayansi ya siasa, aliongeza kuwa hakuna haja ya kuendelea kuogopa, Katiba Mpya inahitajika, hivyo watu waendelee kuipigania kwa mustakabali wa vizazi vijavyo.

“Harakati huwa hazifi, huwezi kuua mawazo, hamna namna ya kuua mawazo ya watu, hata kama watakufa, yale mawazo ya kutaka Katiba Mpya yataendelea kuwepo,” alisema msomi huyo na kuongeza kuwa kupatikana kwake ni suala la muda tu.

Si huyo tu, hata msomi mwenzake, Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikuwa na mawazo yanayoshabihiana na mtazamo huo, akisema Serikali haiwezi kutekeleza dhana ya utawala bora bila kuwa na Katiba bora inayotoa fursa hiyo.

Alisema hamasa ya kudai Katiba Mpya imekuwa kubwa kwa sababu mchakato wake ulishaanza na ukaishia njiani, hivyo, watu mbalimbali wana kiu ya kuona mchakato huo unakamilishwa na nchi inapata Katiba Mpya.

“Nakubaliana na kauli ya Warioba na ukiona wadau wote wanazungumzia suala hilohilo la Katiba Mpya ujue kwamba inahitajika, ni suala la kukubaliana na kupanga namna ya kuitengeneza,” alisema.

Dk Mbunda alisema wadau wamekuwa wakidai Katiba Mpya kwa kuangalia zaidi masilahi yao, hata hivyo, alisema ni muhimu zaidi kuangalia na masuala yanayowagusa wananchi moja kwa moja.

“Moja ya mambo yanayohitaji mabadiliko ni kupunguza madaraka ya Rais, kwa mfano Rais amepewa mamlaka ya kufanya teuzi mbalimbali mpaka kwenye Serikali za mitaa, lakini kimsingi, uteuzi kwenye ngazi ya Serikali za mitaa ulitakiwa kufanywa na mamlaka nyingine katika eneo husika,” alisema.

VIONGOZI WA DINI WAGUSWA.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka alisema Katiba Mpya inahitajika, lakini matamanio ya viongozi wa dini ni kuona wadau wanatumia majukwaa halali ya kuzungumzia suala hilo na kwa lugha inayofaa.

Alisema wangependa kuona viongozi wa kisiasa wakitumia majukwaa halali kujadili suala la mabadiliko ya Katiba kama vile Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Bunge na mikutano mikuu ya vyama vyao.

“Umuhimu wa kupata Katiba mpya upo, ndiyo maana mchakato ulianza, iliundwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba. Viongozi wa dini tusichotaka ni kuona majukwaa yasiyo halali yanatumika vibaya kutoa lugha chafu kwa viongozi,” alisema.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza katika andiko lake anasema inapozungumzwa Katiba Mpya, watu wasitazame uzuri na ubaya wa Katiba iliyopo, bali watazame uzuri au ubaya wa katiba inayodaiwa.

0 comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates