Social Icons

NIFA AD

NIFA AD

NIFAAAA

NIFAAAA

Tuesday, July 13, 2021

TANZANIA; RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AMEFANYA MAZUNGUMZO KWA NJIA YA MTANDAO NA RAIS WA BARAZA LA UMOJA WA ULAYA MHE. CHARLES MICHAEL.


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, jana tarehe 12 Julai, 2021 amezungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dodoma ambapo viongozi hao wawili wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Umoja huo.

Mhe. Michel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa hatua mbalimbali anazochukua tangu kushika hatamu ya uongozi na kumhakikishia kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kuwa mshirika muhimu na wa kimkakati wa maendeleo nchini Tanzania na kikanda.

Aidha, Mhe. Michel amempongeza pia kwa jitihada anazochukua kupambana na ugonjwa wa Corona. Vilevile amemueleza kuwa EU tayari inashirikiana na viwanda mbalimbali  vinavyozalisha chanjo barani Afrika kwa kuvijengea uwezo na kuongeza kuwa iwapo Tanzania itahitaji msaada huo EU iko tayari kuisaidia.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameshukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii na kuwekeza katika miradi ya miundombinu kupitia Benki ya Uwekezaji ya EU. Mhe. Rais Samia amesema kuwa Benki hiyo imetoa Euro milioni 50 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege vya mikoani.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 111.5 kwa ajili ya kuboresha miradi ya sekta ya nishati hususani  matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani  mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha usalama wa chakula.

Mhe. Rais Samia amesema kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemhakikishia Mhe. Michel kuwa utawala wake utasimamia na kuimarisha  demokrasia, utawala bora na haki za msingi za binadamu.

Kuhusu mapambano dhidi  ya ugonjwa wa Corona, Mhe. Rais Samia amemtaarifu Rais huyo wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU) Mhe. Michel kuwa Tanzania tayari imeshajiunga na Mpango wa Kimataifa wa ugawaji wa chanjo kwa nchi masikini (COVAX facility) na ina Mpango wake wa taifa wa kupambana na Corona unaoainisha mahitaji ya nchi hivyo itawasilisha mahitaji yake kwa EU  ili kupata msaada.

Mhe. Rais ameshukuru kupokea mualiko wa kutembelea Umoja wa Ulaya na kumtumia salamu Rais wa Umoja huo Mhe. Bi Ursula von der Leyen.

0 comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates