Wazambia wanaamua leo ikiwa wanataka kumchagua tena Rais wao Edgar Lungu ama mpinzani wake mkuu, Hakainde Hichilema baada ya matokeo mabaya ya uchumi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa na ukandamizaji dhidi ya wapinzani ambao umeibua hofu ya kuzuka machafuko.
Hichilema mwenye umri wa miaka 59, amewahi kushindwa mara mbili na Lungu, mara ya kwanza katika uchaguzi wa 2015 baada ya kifo cha rais wa zamani Michael Sata na katika uchaguzi mkuu uliofuata mwaka mmoja baadaye.
Lungu alilituma jeshi kuzima machafuko yaliyoibuka baada ya makabiliano kati ya wafuasi wa vyama vianvyohasimiana kuelekea uchaguzi wa leo wa rais na bunge, hatua iliyokosolewa na wakosoaji kama mbinu ya kuwatisha na kuwahujumu wapigaji kura wafuasi wa upinzani. Msemaji wa chama cha rais Lungu cha Patriotic Front, PF, Antonio Mwanza, alidai siku ya Jumanne kwamba upinzani unatumia machafuko kuvuruga na kufuja mchakato wa uchaguzi na kuwatisha watu ili wasijitokeze kwa wingi kutumbukiza kura zao kwenye masanduku vituoni.
Wachambuzi wanasema matokeo ya uchaguzi huu unaoshuhudia wagombea wakipambana kwa karibu na kukaribiana, yatatoa muelekea kwa uwekezaji katika nchi hiyo yenye utajiri wa shaba, ambako zaidi ya nusu ya wakazi wake milioni 17 wanaishi katika hali ngumu ya umasikini.
Utafiti umebainisha kuwa hali ngumu ya kiuchumi imepunguza umaarufu na uungwaji mkono wa Lungu, anayetuhumiwa kwa kuchukua mikopo mikubwa bila mpango kufadhili miradi ya kifahari ya ujenzi wa miundombinu, huku kwa upande mwingine gharama za maisha zikipanda.
Katika mji mkuu Lusaka, ilani za rangi ya kijani ya chama cha Lungu cha Patriotic Front zimechukua nafasi kubwa kwenye mabango yaliyowekwa kando kando ya barabara mpya na madaraja ya juu. Wapigaji kura wa upinzani, ambao rangi ya chama chao ni nyekundu, wametulia bila kuonyesha hamasa kubwa katika mji huo ambao ni ngome ya chama cha Patriotic Front. Baadhi yao hata wanavaa nguo za rangi ya kijani ili kuepuka kutumbukia kwenye matatizo, katika kile kinachofahamika kama "mbinu ya matikiti maji".

0 comments:
Post a Comment