Friday, July 16, 2021
TALIBANI YAPENDEKEZA KUSITISHA VITA KWA MIEZI MITATU.
Kundi la Taliban limependekeza kusitisha mapigano kwa muda wa miezi mitatu kwa masharti kuwa serikali itawaachia huru wafungwa 7,000. Kundi hilo linaendeleza mashambulizi makali kote nchini humo.
Mjumbe mmoja kati ya wajumbe wa serikali wanaoshiriki kwenye mazungumzo ya amani na Wataliban, Nader Nadery, ameongeza kuwa waasi hao pia wamedai kuondolewa kwa viongozi wao kwenye orodha ya majina ya wakosaji ya Umoja wa Mataifa.
Haikubainika mara moja ni kwa namna gani serikali itajibu pendekezo hilo la kusitisha mapigano, ambalo limetolewa wakati ambapo Marekani inaongeza kasi ya kuviondoa vikosi vyake, katika mchakato unaotazamiwa kukamilika Agosti 31.
Wakati huo huo vikosi vya usalama vya Pakistan vimetumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya watu waliojaribu kuingia nchini humo kwa nguvu, kutoka Chaman hadi mpaka wa Spin Boldak nchini Afghanistan. Mpaka huo ulifungwa jana na mafisa wa Pakistan baada ya Taliban kuiteka Spin Boldak na kupandisha bendera zao mjini humo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

0 comments:
Post a Comment