Maelfu ya raia wa Cuba wamejumuika katika maandamano makubwa kuwahi kufanyika kwa miongo dhidi ya serikali ya kikomunisti. Picha za mitandao ya kijamii yanaonesha kuwa vyombo vya usalama vinawapiga na kuwashikilia baadhi ya waandamanaji.
Wameandamana mijini, ukiwemo mji mkuu Havana wakiimba na kupaza sauti kuishutumu serikali wanayoitaja ya kidikteta na kutaka uhuru. Wacuba wameghadhabishwa na kuporomoka kwa uchumi, kubanwa kwa uhuru na haki za kiraia na jinsi maafisa nchini humo wanavyolishughulikia janga la Corona.
Waandamanaji hao wanataka mpango wa utoaji wa chanjo kuharakishwa baada ya Cuba kuripoti zaidi ya wagonjwa elfu saba wa maambukizi ya Corona kwa siku na vifo visivyopungua 47 jana Jumapili.
Mwaka jana, uchumi wa Cuba ambao kwa kiasi kikubwa unadhibitiwa na serikali ulipungua kwa asilimia kumi na moja ukitajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Uchumi huo unasemekana umeathirika vibaya hivyo kutokana na janga la Corona na vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya taifa hilo.
Maelfu ya wafuasi wa serikali pia wameandamana baada ya rais kuwahimiza kulinda mapinduzi wakiangazia maandamano ya kutaka ukombozi yaliyofanyika mwaka 1959 na kupelekea utawala wa Kikomunisti Cuba. Rais Miguel Diaz Canel amesema maandamano hayo ni uchochezi kutoka kwa mamluki anaodai wamekodishwa na Marekani kuliyumbisha taifa hilo.
Akilihutubia taifa kupitia televisheni Rais Canel amesema maagizo ya kuanza mapambano mitaani yashatolewa kwa wanamapinduzi ili kulilinda taifa. Mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani katika Amerika ya Kusini Julie Chung ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wanatiwa wasiwasi mkubwa na wito huo wa mapambano na kuongeza kuwa wanawaunga mkono raia wa Cuba wanaotaka kuandamana kwa amani lakini wakati huo huo wanatoa wito wa kuwepo utulivu na kulaani ghasia za aina yoyote.
Mmoja wa waandamanaji hao aliyejitambulisha kwa BBC kama Geovanis Gonzalez amesema hawawezi tena kustahimili ugumu wa maisha kwani hawana chakula, dawa wala uhuru. ''Tuko hapa kwasababu ya kupinga ukandamizaji dhidi ya watu. Wanatunyima chakula ili tufe. Havana inaporomoka. Hatuna makazi, hatuna chochote lakini wana fedha za kujenga mahoteli na sisi twafa njaa "
Maandamano ya kupinga serikali yalianzia mjini San Antonio de los Banos kusini magharibi mwa mji mkuu Havana lakini muda mfupi yalisambaa kote nchini humo. Watu walitumia mitandao ya kijamii kuonesha moja kwa moja kwa moja maandamano hayo huku waandamanaji wakimshutumu vikali sana.



0 comments:
Post a Comment