Na. John Mapepele
Rais
wa Jamhuri ya Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kuelekea kilele cha
maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru leo Disemba 9, 2021 amesema Tanzania
imepiga hatua kubwa kwenye lugha ya Kiswahili.
Rais Samia
ameyasema haya jana usiku Disemba 8, 2021 jijini Dar es Salaam wakati
akiwahutubia wananchi ambapo alieleza pamoja na mambo mengine mafanikio
yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania.
“Nchi
nyingi zinatumia lugha za kigeni kama lugha za mataifa yao
zinazowaunganisha, inapendeza kuona kuwa tunatimiza miaka 60 tukiwa
wamoja wenye utambulisho mmoja na lugha moja ya Kiswahili inayoendelea
kupata umaarufu kimataifa siku hadi siku”. Amefafanua Rais Samia.
Amesema
wakati Tanzania ilipopata uhuru Kiswahili haikuwa lugha inayozungumzwa
na watu wote ndani ya Tanganyika bali kizazi kilichofuata baada ya uhuru
walijifunza kiswahili shuleni. Hii inafanya nchi kuwa kati ya nchi
chache zenye lugha ya taifa yenye asili ya nchi husika.
Ameongeza
kuwa katika miaka 60 Tanzania imefanikiwa kushawishi Kiswahili kuwa
moja ya lugha rasmi zinazotumika katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika na Umoja wa Afrika.
Amesema,
Shirika la Umoja wa Mataifa Sayansi na Elimu (UNESCO) limepitisha
azimio la kutenga siku ya tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya
Kiswahili duniani ambapo amesema azimio hilo linaifanya lugha ya
Kiswahili kuwa kuwa ya kwanza katika bara la Afrika kutambuliwa na
kutengewa siku yake rasmi.
0 comments:
Post a Comment