Thursday, August 19, 2021
GARI LA JWTZ LAGONGANA NA LORI, WATU 10 WAFARIKI
AJALI mbaya imetokea na kuua watu 10 huku wengine 8 wakijeruhiwa baada ya gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kugongana uso kwa uso na gari la mizigo katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Ajali hiyo imetokea leo Jumatano 18, 2021 katika Kijiji cha Ilalwe, Kata ya Bukombe wilayani Bukombe na kuhusisha gari la jeshi aina ya Leyland Ashok lenye namba za usajili JW 12 lililokuwa limebeba ndugu waliotoka kwenye msiba wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kugongana na lori la mizigo aina ya Scania lenye namba za usajili T 130 DRZ.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amesema majeruhi 6 wamewahishwa katika Hospitali ya Ushirombo na wawili wapo kituo cha afya Masumbwe wakiendelea kupatiwa matibabu huku chanzo cha ajali hiyo kikiwa hakijafahamika.
DC Nkumba amesema mpaka sasa taarifa aliyopokea miongoni mwa marehemu yupo askari mmoja wa jeshi la wananchi.
Aidha, miili ya marehemu waliofariki kutokana na ajali hiyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Masumbwe na jeshi la polisi linandelea na uchunguzi zaidi kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment